BIBLEPAGE.NET

Someni Neno la Mungu juu ya Internet

Aya ya Siku

Baada ya hayo Yesu akamkuta ndani ya hekalu, akamwambia, Angalia, umekuwa mzima; usitende dhambi tena, lisije likakupata jambo lililo baya zaidi

Yohana 5:14


 

Sura ya 401Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
2Siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza utaisimamisha hiyo maskani ya hema ya kukutania.
3Nawe utatia ndani yake sanduku la ushuhuda, nawe utalisitiri hilo sanduku kwa pazia.
4Nawe utaleta meza na kuitia ndani, na kuviweka sawasawa vile vitu juu yake; kisha utakileta ndani kile kinara cha taa, na kuziwasha taa zake.
5Kisha utaisimamisha madhabahu ya dhahabu kwa kufukizia uvumba mbele ya sanduku la ushuhuda, na kulitia pazia mlangoni mwa hiyo maskani.
6Kisha utaweka madhabahu ya kuteketeza sadaka mbele ya mlango wa maskani ya hema ya kukutania.
7Kisha utaliweka birika kati ya hema ya kukutania na hiyo madhabahu, nawe utatia maji ndani yake.
8Kisha utausimamisha ukuta wa ua kuuzunguka pande zote, na kuitundika sitara ya lango la ua.
9Kisha utayatwaa mafuta ya kutiwa, na kuitia mafuta hiyo maskani, na kila kitu kilicho ndani yake, na kuiweka iwe takatifu, na vyombo vyake vyote; nayo itakuwa takatifu.
10Kisha utaitia mafuta madhabahu ya kuteketeza sadaka, na vyombo vyake vyote; na kuiweka takatifu madhabahu; na hiyo madhabahu itakuwa takatifu sana.
11Kisha utalitia mafuta birika na tako lake, na kuliweka liwe takatifu.
12Kisha utamleta Haruni na wanawe hapo mlangoni pa hema ya kukutania, nawe utawaosha kwa maji.
13Kisha utamvika Haruni mavazi matakatifu; nawe utamtia mafuta, na kumweka awe mtakatifu, ili apate kunitumikia katika kazi ya ukuhani.
14Kisha utawaleta wanawe, na kuwavika kanzu zao;
15nawe utawatia mafuta kama ulivyomtia mafuta baba yao, ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani; na huko kutiwa mafuta kwao kutakuwa ni kwa ukuhani wa milele katika vizazi vyao vyote.
16Musa akafanya hayo yote; kama yote Bwana aliyoagiza ndivyo alivyofanya.
17Hata mwezi wa kwanza wa mwaka wa pili, siku ya kwanza ya mwezi ile maskani ilisimamishwa.
18Musa akaisimamisha maskani, akayaweka matako yake, akazisimamisha mbao zake akayatia mataruma yake, akazisimamisha nguzo zake.
19Akaitanda hema juu ya maskani, akakitia kifuniko cha hema juu yake; kama Bwana alivyomwamuru Musa.
20Akautwaa ule ushuhuda, akautia ndani ya sanduku, akaiweka miti ya kuchukulia juu ya sanduku, akakiweka kiti cha rehema juu ya sanduku;
21kisha akalileta sanduku akalitia ndani ya maskani, naye akalitundika pazia la sitara, akalisitiri sanduku la ushuhuda; kama Bwana alivyomwamuru Musa.
22Akaitia meza ndani ya hema ya kukutania, upande wa maskani ulioelekea kaskazini, nje ya pazia.
23Akaipanga ile mikate juu yake mbele za Bwana; kama Bwana alivyomwamuru Musa.
24Kisha akakitia kinara cha taa ndani ya hema ya kukutania, kuikabili ile meza, upande wa maskani ulioelekea kusini.
25Kisha akaziwasha taa zake mbele za Bwana, kama Bwana alivyomwamuru Musa.
26Akaitia madhabahu ya dhahabu ndani ya hema ya kukutania mbele ya pazia.
27Akafukiza juu yake uvumba wa manukato kama Bwana alivyomwamuru Musa.
28Akalitia pazia la mlango wa maskani.
29Akaiweka madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa mlangoni pa maskani ya kukutania, akatoa sadaka ya kuteketezwa juu yake, na sadaka ya unga; kama Bwana alivyomwamuru Musa.
30Akaliweka birika kati ya hema ya kukutania na madhabahu, akatia maji ndani yake ya kuoshea.
31Musa na Haruni, na wanawe wakanawa mikono yao na miguu yao ndani yake;
32hapo walipoingia hema ya kukutania, na hapo walipoikaribia madhabahu walinawa kama Bwana alivyomwamuru Musa.
33Akausimamisha ukuta wa ua kuizunguka maskani na madhabahu, akalitundika pazia la mlango wa ule ua. Basi Musa akaimaliza hiyo kazi.
34Ndipo lile wingu likaifunikiza hema ya kukutania, na huo utukufu wa Bwana ukaijaza maskani.
35Wala Musa hakuweza kuliingia hema la kukutania, kwa sababu lile wingu lilikaa juu yake, na huo utukufu wa Bwana ukaijaza maskani.
36Na hapo lile wingu lilipoinuliwa kutoka juu ya maskani, wana wa Israeli wakaenda mbele katika safari zao zote,
37bali kama lile wingu halikuinuliwa, wakati ule hawakusafiri hata siku ile lilipoinuliwa tena.
38Kwa maana lile wingu la Bwana lilikuwa juu ya maskani wakati wa mchana, na mlikuwa na moto ndani yake wakati wa usiku, mbele ya macho ya nyumba ya Israeli katika safari zao zote. • Matoleo mengine  
 • English
 • Français
 • Deutsch
 • Español
 • Português
 • Italiano
 • Nederlands
 • Român
 • Dansk
 • Svensk
 • Suomi
 • Norsk
 • Čeština
 • русский
 • Український
 • Български
 • Polski
 • Hrvatski
 • Magyar
 • Shqiptar
 • עברית
 • Türk
 • 圣经
 • 聖經
 • 한국의
 • 日本語
 • Tiêng Viêt
 • ภาษาไทย
 • Tagalog
 • Indonesia
 • हिन्दी
 • தமிழ்
 • ਪੰਜਾਬੀ
 • اردو
 • Somali
 • Kiswahili
 • العربية